Wednesday, October 10, 2012


SERIKALl inaonekana haitaki tena mchezo katika taasisi zake na hivyo imeamua kuchukua uamuzi mzito kwa kuendelea kusimamisha kazi wakuu wa taasisi hizo ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma mbalimbali. Hatua hizo zinalenga kuondoa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi dhidi ya utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi hao, lakini pia ikitafuta kujiridhisha kwa kuthibitisha tuhuma hizo kwa ushahidi usio na shaka. Lengo pia ni kuhakikisha kila mtu anatendewa haki na hakuna anayeonewa na hatimaye utendaji kazi serikalini na katika taasisi zake unakuwa wa kuridhisha. Wimbi la viongozi hao kusimamishwa liliendelea jana, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya alisimamishwa kazi kwa tuhuma za ununuzi wa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV). Mbali na Mgaya, wengine waliosimamishwa pamoja naye ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Sadiki Materu na Ofisa Udhibiti wa Ubora, David Masero. Mgaya anakuwa kiongozi wa sita wa taasisi nyeti nchini kusimamishwa kazi kwa tuhuma hizo kwa mwaka huu. Serikali pia kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imesitisha uzalishaji wa dawa zote katika kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) hadi uchunguzi unaofanywa kupitia vyombo vya usalama kuhusu uzalishaji wa dawa bandia utakapokamilika kwa hatua zaidi za kisheria. Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema tuhuma za MSD kununua dawa bandia kutoka TPI ziligundulika baada ya matokeo ya ukaguzi, ufuatiliaji na uchunguzi wa kimaabara. Alisema mwanzoni mwa Agosti, Wizara kupitia TFDA kwa kuzingatia Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ilibaini kuwapo ARVs bandia aina ya TT-VR 30 toleo namba OC.01.85 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara. Baada ya kubainika kwa tatizo hilo, Dk Mwinyi alisema Wizara kupitia TFDA ilifanya ukaguzi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na baadaye ukaguzi wa kina katika mikoa mingine nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama. “Ukaguzi huu ulifanyika kati ya Agosti 6-31 mwaka huu na ulihusisha MSD makao makuu na kanda pamoja na kiwanda cha TPI ambacho ndicho kilitengeneza dawa hiyo. Pia sampuli za dawa husika zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara,” alisema. Alisema baada ya kubaini tatizo hilo, waliwataarifu waganga wakuu wa mikoa yote nchini na kuwaelekeza wasimamishe matumizi ya ARVs toleo namba OC.01.85 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mikoa yao. Mbali na kusitisha matumizi, waganga hao walielekezwa kuiondoa dawa hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuirudisha kwa msambazaji ambaye ni MSD na Wizara kupitia TFDA ilifanya uchunguzi wa kimaabara ili kuainisha viambata vya dawa hiyo. Dk Mwinyi alisema katika ukaguzi na ufuatiliaji huo pamoja na uchunguzi wa kimaabara, walibaini kwamba dawa yenye jina la biashara TT-VIR 30 toleo namba OC.01.85 ni bandia kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi . “Nyaraka zilizopo zinaonesha kuwa kiwanda cha TPI waliiuzia MSD dawa hiyo bandia na ilitengenezwa Machi mwaka jana na muda wake wa matumizi unakwisha Februari 2013,” alisema Dk Mwinyi. Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, dawa hiyo bandia ilikuwa na rangi mbili tofauti ambazo ni njano na nyeupe; zilizokuwa na rangi ya njano zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine vilivyopaswa kuwepo. “Vidonge vyenye rangi nyeupe vilikuwa na viambata vinavyotakiwa kuwepo yaani Niverapine. Vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikutwa tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA,” alisema. Hatua mbadala Dk Mwinyi alisema Wizara itahakikisha kuwa ARVs zipo za kutosha na zenye ubora unaotakiwa na zitaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Aliwakumbusha waganga wakuu wa wilaya na mikoa kuimarisha kamati za dawa na tiba katika vituo vya huduma za afya, ambazo zina majukumu ya kusimamia upokeaji, uhakiki wa ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba. Pia alisema matarajio ya wizara ni kuendelea kuimarisha mfumo na taratibu za uhakiki wa ubora, utunzaji, usambazaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Alitoa rai kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwapo dawa zenye ubora wenye shaka au uvunjifu wa sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa. Alihimiza wananchi kuendelea kutumia ARVs kwa kuwa dawa hiyo yenye shaka imekwishaondolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Hata hivyo, waandishi walipotaka kufahamu endapo kuna wananchi waliojitokeza kutokana na athari za dawa hizo, Dk Mwinyi alisema mpaka sasa hajapokea ripoti yoyote na uchunguzi umefikia katika hali nzuri na hivi karibuni utakamilika. Pia alisema mpaka sasa wamerudisha makopo 9,570 ya dawa hizo bandia na makopo 2,600 yanaendelea kukusanywa na kurudishwa. Waliosimamishwa kabla Mei 18, Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili ikiwamo ya kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi. Juni 5, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Paul Chizi alisimamishwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kutokana na ukiukwaji wa sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2003 kifungu 17(1) au (3). Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, alisimamishwa kazi Julai 14 kupisha uchunguzi juu ya tuhuma dhidi yake za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Julai 19, Bodi ya Wakurugenzi wa benki ya NBC ilimlazimisha Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki hiyo, Lawrence Mafuru kwenda likizo ili kupisha uchunguzi juu ya ubadhirifu. Hata hivyo baada ya uchunguzi, Mafuru hivi karibuni alirejeshwa kazini baada ya Bodi kuridhika kuwa hakufanya ubadhirifu wowote. Agosti 23, Waziri wa Uchukuzi Dk Mwakyembe alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Ephrahim Mgawe na wasaidizi wake wawili ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

BREAKING NEWS:- Soko la UYOLE MBEYA Linateketea kwa moto


BREAKING NEWS:- Soko la UYOLE MBEYA Linateketea kwa moto Soko la Uyole mkoani Mbeya linateketea kwa moto, jitahada za kuuzima zinaendelea, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana