WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amekanusha uvumi uliosambaa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa ametangaza vita na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Bw. Edward Lowassa kama atachukua fomu ya kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote bali ni za kutungwa kwani hajawahi kuzungumza lolote juu ya Bw. Lowassa, wala kuzungumza na mtu yeyote kuhusu jambo hilo.
Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari ili kufafanua masuala mbalimbali likiwamo suala la rushwa katika uchaguzi wa kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Jimbo la Hanang', mkoani Manyara.
Alidai kushangazwa na jinsi habari hizo zilipotokea na akawataka waandishi wa habari kuwa makini na wasikubali kutumiwa na wanasiasa wanaosaka urais 2015.
“Kuna baadhi ya magazeti yaliandika Sumaye kulipua bomu, mengine Sumaye kupasua jipu na kibaya zaidi, hivi majuzi gazeti moja likaandika Sumaye atangaza vita na Lowassa, ninachosema mimi sina jipu wala bomu la kulipua.
“Mimi sina ugomvi na Lowassa, hata nikiamua urais 2015 sitafanya hivyo kwa ajili ya mtu bali kwa masilahi ya Taifa,” alisema.
Kuteta na CHADEMA
Bw. Sumaye pia alishangazwa na habari iliyoandindwa na gazeti moja (bila kukitaja jina), kikidai alitetea (kufanya mazungumzo), na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Sijawahi kuzungumza na CHADEMA kuhusu kuhamia chama chao, hata kama ningetunana nao, ufike wakati wapinzani wasionekane kama maadui.
“Habari hiyo ni ya kutengeneza pamoja na picha iliyowekwa mbele ya gazeti nikiwa na Mbowe ili nionekane nateta naye, namuomba Mwenyezi Mungu jambo hili lifahamike ni uvumi tu ili tusije tukaiingiza nchi katika matatizo,” alisema Bw. Sumaye.
Uchaguzi NEC Hanang'
Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, katika Jimbo la Hanang', Bw. Sumaye alisema alipoteza nafasi hiyo kwa sababu uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa hivyo kumuathiri kwa
kiasi kikubwa.
Alisema mbali wajumbe kupewa rushwa pia yalikuwepo makundi aliyoyahita ya 'kiharamia', ambayo yalikuwa yakiwahamisha wajumbe nyakati za usiku ili wasipige kura.
“Mambo yaliyotokea Hanang', yalijitokeza sehemu nyingi lakini tofauti ni kwa ukubwa gani na nani yalimkuta,” alisema.
Aliongeza kuwa, pamoja na kwamba vitendo vya rushwa vilikuwepo siku za nyuma, safari hii hali ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya mitandao iliyokuwa ikisambaza fedha katika maeneo mbalimbali ili kuwang'oa wanasiasa hasa wanaokemea maovu.
Alisema zamani watu walikuwa wakienda wenyewe na kutoa fedha kwa wakazi wa eneo husika ili wachaguliwe lakini sasa hali hiyo imebadilika ambapo baadhi ya watu aliodai kuwa wanasaka urais kinguvu, wamejenga mtandao wa kununua wapiga kura.
“Kwa sasa kuna mtandao wa kuonga wapiga kura tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mtu alikuwa akienda eneo husika na kuwapa fedha wapiga kura ili wachaguliwe,” alisema Bw. Sumaye akinukuu baadhi ya hotuba alizowahi kuzitoa katika matukio mbalimbali akikemea vitendo vya rushwa.
Hata hivyo, alipobanwa na waandishi wa habari kama anaweza kuutaja mtandao huo na eneo ambalo wajumbe walipewa rushwa Bw. Sumaye alikataa kata kata kuzungumzia zaidi suala hilo.
“Pamoja na kufanyiwa vitendo hivi, sitafikisha malalamiko yangu katika vikao vya chama wala kukata rufaa kwani yaliyojitokeza yalikuwa yakifahamika pia itaonekana nipo ndani ya CCM
kwa ajili ya vyeo.
“Mimi ni mwana CCM, nina imani na chama changu ambacho kiliunganishwa na vyama vya TANU na ASP, sipo ndani ya chama kwa ajili ya kutaka vyeo,” alisema Bw. Sumaye na kuongeza;
“Rushwa haizalishwi na demokrasia bali tunaizalisha wenyewe kwa sababau zetu za kijinga, nchini Marekani na Uingereza kuna demokrasia, mbona hatusikii vitendo hivi,” alihoji Bw. Sumaye.
Alisema kama wapiga kura wasipokuwa makini, Taifa litaambulia viongozi waliochaguliwa kwa nguvu za fedha badala ya utashi wa wananchi wenye haki ya kuchagua kiongozi wanayempenda.
Bw. Sumaye alisema katika nchi zenye demokrasia, wapiga kura huchagua kiongozi wanayempenda na mwenye uwezo lakini katika nchi zilizopondeka kwa rushwa, fedha ndio inayochagua viongozi
na kazi ya wapiga kura ni kupiga mihuri tu.
Alihadharisha hali hiyo na kudai kuwa, nchi nyingi zimeingia katika machafuko kutokana na chaguzi za aina hiyo na kushauri wale wanaopiga kelele kukemea vitendo hivyo vya rushwa waungwe mkono badala ya kusakama.
Aliwashauri viongozi ndani ya CCM, wajirekebishe kabla wananchi hawajachoshwa na hali hiyo na kuamua kuingia mitaani.
“Wananchi watachoshwa na hali hii, hawawezi kuvumilia mambo haya kama yataendelea ipo siku watasema inatosha, wakifikia hatua hiyo hali itakuwa mbaya zaidi,” alisema.
Kuteteleka kisiasa na hatma ya kuwania urais 2015
Bw. Sumaye aliulizwa kuanguka kwake NEC, pengine pamemfanya ateteleke kisiasa na kuathirika katika mbio za kuwania urais 2015, ambapo akijibu swali hilo alisema, hali hiyo imemuongezea nguvu na akaahidi kuendeleza mapambano akiwa ndani ya CCM.
“Kuangushwa kwangu ujumbe wa NEC kumenipa nguvu zaidi, wala sijateteleka kisiasa bali nitaendelea kupambana na maovu nikiwa ndani ya chamachangu CCM,” alisema Bw. Sumaye.
Alisema hata akiamua kuwania urais 2015, ingawa bado hajatangaza dhamira hiyo, matokeo hayo yamemrahisishia njia kwani kama angepata ujumbe wa NEC, ingemuwia vigumu kujitosa katika
mbio hizo.