Wednesday, September 12, 2012

'Serikali isiiogope Malawi'


SERIKALI imetakiwa kuwa makini katika kushughulikia mgogoro uliopo na Malawi kuhusu mpaka ndani ya Ziwa Nyasa na kutokubali kuliachia ziwa hilo kutokana na umuhimu wake kwa uchumi.

Akizungumza katika kikao kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na wazee wa Mji Mdogo wa Lituhi wilayani Nyasa, mmoja wa wazee hao, Conrad Chale alisema, Serikali haipaswi kuogopa wala kuliachia Ziwa Nyasa kwani mpaka uko ndani ya ziwa na si nje kama Malawi inavyodai.

Alisema madai hayo ya Wamalawi hayana msingi wala ukweli wowote kwani kabla na baada ya nchi hiyo kupata uhuru, karibu huduma zote za muhimu walikuwa wakipata Tanzania na kuishi nao kama ndugu moja huku wakitambua uwepo wa mpaka katikati ya ziwa.

Chale alisema Wamalawi ndiyo wanaotakiwa kuilipa Tanzania baada ya kupata huduma nyingi za kijamii kutoka nchini hasa wale wanaoishi kando kando ya ziwa ilo.

Alisema Serikali ya Malawi haipaswi kung’ang’ania kuwa ziwa hilo ni lake kwani upo ushahidi wa kutosha unaoonesha uwepo kwa mpaka wa nchi hizo mbili katikati ya ziwa na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu mpaka huo ili kuepusha nchi hizo kuingia vitani na kusababisha madhara kwa wananchi.

Aliiomba serikali, kulinda mpaka huo kwa gharama ikiwemo rasilimali zilizopo katika ziwa hilo ambalo ndiyo tegemeo pekee la uchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.

Waziri Membe alisema Serikali itaendelea kutafuta muafaka wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania ndiyo maana imekwenda kwa wazee waliokuwepo katika maeneo hayo kwa muda mrefu, ili kupata ushahidi kuhusu madai ya nchi ya Malawi.

Waziri Membe ambaye aliongoza ujumbe wa wataalamu mbalimbali katika ziara hiyo, aliwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na kutokuwa na wasi wasi kwani tatizo hilo linashughulikiwa na ikibidi watafika hadi mahakama ya kimataifa kutafuta haki ya Watanzania.

Alisema Malawi wanatafuta sifa mbele ya jumuiya ya kimataifa, lakini haitafanikiwa kwani wanafahamu ukweli juu ya mpaka huo na uhalali wa Serikali ya Tanzania kumiliki sehemu ya Ziwa Nyasa.

Aliwashukuru wazee wa wilaya hiyo kwa kuunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kutafuta namna ya kumaliza mgogoro huo na uwepo wa wazee hao ambao umesaidia kupata ukweli.

Wakati huohuo, Serikali imeombwa kuboresha huduma mbali mbali za jamii kwa wananchi waishio kando ya ziwa Nyasa, ili kupunguza kero kubwa za muda mrefu zinazowakabili wananchi hao zinazosababishwa na ukosefu wa miundombinu.

Akitoa kilio chao mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, mmoja wa wakazi wa Liuli, Raphael Kambanga alisema kukosekana kwa miundombinu ya kisasa ni moja ya sababu zilizoifanya Wilaya ya Nyasa kubaki masikini licha ya kuwepo kwa rasilimali za kutosha.

Kambanga alimueleza Waziri Membe kuwa hivi sasa bidhaa nyingi zinazotumiwa na wananchi wa Nyasa zinatoka Malawi na Msumbiji jambo ambalo ni hatari kwa uchumi.

Alifafanua kuwa uhusiano huo wa kibiashara na nchi jirani, unaikosesha Serikali mapato ya kutosha kutokana na kodi za kuingiza bidhaa huku wafanyabiashara wajanja wakitumia mwanya huo kufanya biashara za magendo.

Alisema wanalazimika kutumia muda mwingi kufuata huduma za jamii mbali huku muda wa kufanya shughuli za maendeleo ukipita, kitu ambacho ni hatari kubwa kwa kuwa wanashindwa kufanya kazi zinazoweza kupunguza umasikini katika familia zao.

"Tunakuomba pamoja na matatizo tuliyonayo kati yetu na Malawi, mtukumbuke sisi tunaoishi huku pembezoni… hali yetu ni mbaya ndiyo maana hata wenzetu Wamalawi wanatumia nafasi hiyo kuhalalishia mpaka nje ya ziwa kutokana na ukimya wa Serikali yetu," alisema.

Kambanga aliitahadharisha Serikali juu ya mipaka iliyopo ambayo hakuna ulinzi wa kutosha na inaweza kutumika kwa kupita maadui hasa kutoka Malawi na Msumbiji kufanya lolote wanaloweza kwa maslahi ya nchi zao, kwa hiyo ni vizuri serikali kuangalia maeneo hayo mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment