Tuesday, October 9, 2012

Mume ajinyonga kwa kunyimwa unyumba

MKAZI wa Mtaa wa Mpanda Hotel wilayani Mpanda katika Mkoa wa Katavi, Nzego Vicent (33) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani huku akimlalamikia mkewe kwa kumnyima unyumba kwa siku tatu mfululizo bila kupewa sababu zilizomridhisha.

Mashuhuda wakiwemo baadhi ya majirani wa wandoa hao kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, walidai kabla ya kujinyonga, Vicent ambaye alikuwa ametoka kunywa pombe za kienyeji, alifika nyumbani kwake saa 6:20 usiku na kumtaka mkewe ampe unyumba.

Majirani hao walidai kuwa mke wa marehemu, Agnes Nicodemu alilalamikia mumewe kuwa hakuwa tayari kumpatia unyumba kutokana na shughuli alizokuwa amezifanya mchana kutwa na kumsihi avumilie hadi siku itakayofuata kwa kuwa alikuwa amechoka sana.

“Siku mbili mfululizo mama huyo kutokana na kuelemewa na kazi nzito za shamba na nyumbani kwake ambazo alikuwa akizifanya kuanzia alfajiri hadi usiku wa manane, aliendelea kumsihi mumewe ambaye alikuwa akirudi nyumbani usiku kuwa amechoka,“ alidai mama mmoja jirani na wanandoa hao.

Inadaiwa kuwa baada ya Vicent kujibiwa hivyo kwa siku tatu mfululizo hakuridhika na madai hayo ya mkewe ndipo alipoanza kumshutumu kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine.

Inadaiwa siku ya tatu, Vicent alimshambulia mkewe huyo kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake huku akimtolea maneno ya kumtisha kuwa lazima atamuua kwa mapanga iwapo ataendelea kuwa mkaidi katika unyumba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, baada ya kuona kipigo kimezidi mwanamke huyo alikimbia nje ili kukwepa kipigo na mumewe naye alitoka nje ya nyumba yao akiwa ameshikilia mashoka mawili na kwenda kusikojuliakana na kuiacha nyumba ikiwa wazi.

Ilipotimu saa 12:30 alfajiri, mwanamke huyo alifuatwa na majirani waliomweleza kuwa mumewe amejinyonga kwa katani jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi ndipo alipoandamana nao hadi eneo hilo na kumuona akiwa amening’inia juu ya mti.

Nagu naye chali CCM

ILE methali ya mwosha huoshwa imejidhihirisha mkoani Manyara katika mwendelezo wa uchaguzi wa CCM na jumuiya zake.

Hali hiyo imejitokeza kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu, ambaye hivi karibuni ‘alimwosha’ Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye katika uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Wakati maji hayajakauka katika mwili wa Sumaye ambaye juzi alilalamikia uchaguzi huo kugubikwa na rushwa, Dk Nagu naye ‘ameoshwa’ katika kinyang’anyiro cha kutetea nafasi aliyokuwa nayo ya ujumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia mkoa wa Manyara.

Katika uchaguzi huo kati ya kura halali 391 zilizopigwa, Dk Nagu alipata 139 huku mpinzani wake, Martha Umbulla ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Manyara, akiibuka kidedea kwa kupata kura 252.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita, msimamizi wa uchaguzi huo, Ndengasso Ndekubali ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Mkoa, alisema katika uchaguzi huo, kura tisa ziliharibika.

Katika uchaguzi huo wa ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Hanang, ambako Nagu aliibuka kidedea dhidi ya Sumaye, kati ya kura 1,129 zilizopigwa, alipata kura 648 dhidi ya 481 za Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Akizungumza Dar es Salaam juzi na waandishi wa habari, Sumaye alidai kuwa kilichomwangusha katika uchaguzi wa NEC, ni rushwa aliyoiita ya mtandao.

Alidai kuwa uchaguzi huo uliompa Dk Nagu ushindi, uligubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho, uharamia, kuhamishwa kwa wapiga kura usiku na maovu mengine.

Katika uchaguzi wa ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Anna Jorojiki alishinda kwa kupata kura 199 dhidi ya Bahati Moses aliyepata kura 150.

Ndekubali alisema pia aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara kati ya mwaka 2005 na 2010, Dora Mushi, alimwangusha Elizabeth Malley katika nafasi ya Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa, akitetea nafasi hiyo baada ya kuishikilia kwa miaka 10.

Alisema kati ya wanachama wa UWT 400 waliopiga kura za kuchagua Mwenyekiti wa UWT Mkoa, wanachama 17 kura zao ziliharibika na kati ya kura halali 383 zilizopigwa, Mushi alipata 238 na Malley 145.

Akizungumza na waandishi baada ya kushinda nafasi hiyo, Umbulla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, alishukuru wanachama wa UWT kwa kumchagua na kuwataka wavunje kambi na vikundi ili kupanua wigo wa kujenga na kudumisha chama.

Alisisitiza, kwamba hakuna mbinu yoyote aliyotumia kumshinda Dk Nagu ila wanawake hao walikumbuka mambo aliyoyafanya kwenye nafasi yake.

Alisema wanawake wa Manyara wanajua nini amewafanyia kupitia nafasi yake ya ubunge wa viti maalumu na aliwashukuru kwa kumwona kuwa anafaa kwani asingewaelewa wasingemchagua.

Kidato cha nne wakosa mitihani

TAKRIBANI wanafunzi 97 wa sekondari ya Seeke, wilayani Kahama mkoani Shinyanga hawatafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne, kutokana na kukosa fomu za maendeleo ya mwanafunzi akiwa shule ya msingi (TSM 9).

Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wanafunzi hao wakisubiri kuingia katika vyumba vya mitihani. Wakizungumza na gazeti hili, wanafunzi hao walidai fomu hizo walizijaza na kulipa ada ya mitihani na kuongeza kuwa wanashangaa kuona jana wakizuiwa kuingia chumba cha mtihani.

“Aliitwa Mwalimu Mkuu Msaidizi, Daniel Mtuli ambaye alitaja majina ya wanaotakiwa kufanya mtihani huku wengine wakiachwa katika orodha hiyo,” alidai mmoja wa wanafunzi hao.

Alidai katika orodha hiyo, wanafunzi 53 waliochaguliwa kuingia katika chumba cha kufanyia mitihani kati ya wanafunzi 150 wanaotakiwa kufanya mitihani hiyo hali ambayo ilisababisha wanafunzi 97 kutofanya mtihani huo jana.

“Mimi nina siku nne tangu nikabidhiwe ofisi hii na Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kahama, Joseph Gwasa na nilipokabidhiwa, nilipewa maelekezo kuwa ni wanafunzi 53 ndio wanaopaswa kufanya mtihani huo wa kidato cha nne,” alisema Mtuli alipohojiwa kuhusu utata huo.

Mtuli alisema Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Maduhu alisimamishwa kazi katika shule hiyo tangu Oktoba 3 kwa sababu hizo hizo.

Alielezea kusikitika kuona wanafunzi hao wakipoteza muda wao wa miaka minne na kuambiwa jana kuwa hawawezi kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya sekondari.

Wanafunzi hao walipofika katika ofisi ya Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya, kujua hatima yao ya kufanya mitihani, hawakuonana naye kwa madai kwamba alikuwa na kazi nyingi.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao waliamua kuandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya kupinga kitendo cha kuzuiwa kufanya mitihani. Juhudi za kumpata Mpesya kwa njia ya simu ili kujua hatma ya wanafunzi hao, zilishindikana kwa kuwa simu yake ilikuwa haipatikani.

Wakati hayo yakitokea Shinyanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Joyce Ndalichako, alisema mitihani hiyo ya kidato cha nne, ilianza vizuri bila matatizo na wanafunzi hao jana walianza na masomo ya Uraia na Kiingereza.

“Ni mapema mno kuzungumzia hali halisi, lakini mpaka sasa mambo ni mazuri ingawa baadaye kupitia taarifa za wasimamizi, tunaweza kukuta taarifa za udanganyifu na mambo mengine ya changamoto,” alisema Dk Ndalichako.

Gazeti hili lilitembelea baadhi ya shule za Dar es Salaam zikiwamo za Salma Kikwete, Manzese, Jitegemee na Makongo na kukuta wanafunzi wakifanya mitihani yao kwa utulivu huku wasimamizi wakidai kutokuwapo na mushkeli wowote.

Hata hivyo, katika sekondari ya Manzese Mkuu wa Shule, aliyekataa kutaja jina lake aliwajia juu waandishi wa habari kwa kuingia ndani ya shule hiyo na kuhoji hali ya mitihani huku akidai kuwa hiyo si kazi yao kama wanataka kujua wakamwulize Ndalichako.

“Nasema hivi, mimi sijui mmefuata nini? Mnaniuliza mimi kwani mimi ndiye nafanya mtihani, kasubirini huko kwa Mkurugenzi wa Elimu au kwa Ndalichako hapa hamruhusiwi,” alisema kwa jazba.