Friday, October 12, 2012

ARVs bandia zazua balaa


TAARIFA za kusambazwa kwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) ambazo ni bandia, zimesababisha baadhi ya wananchi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU), kutupa dawa zao na kusitisha kuzitumia.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imeitaka Serikali baada ya uchunguzi kuhusu utengenezwaji na usambazwaji wa dawa hizo, watakaothibitishwa kuhusika washitakiwe na kuchukulia hatua kali za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lediana Mung’ong’o, alisema baada ya Kamati yake kupata taarifa za kusambazwa kwa dawa hizo, ilikutana na wadau kujua hali halisi ikabaini kuwa waathirika wengi wameacha kutumia dawa hizo.

“Jamani tuna taarifa kuwa wenzetu hawa, kwa hofu wametupa dawa zao na wengine wamesitisha kabisa kuzitumia, natoa mwito kwao kurejea kwenye dawa zao, kwa kuwa Serikali imetuhakikishia dawa sahihi zipo,” alisema Mung’ong’o.

Alisema hata hivyo dawa hizo bandia zilisambazwa katika mikoa michache ya Mwanza, Iringa na Tanga na kuwatoa wasiwasi wanaozitumia, kwamba Serikali inafuatilia ili kubaini wagonjwa waliozitumia na kuwasaidia.

Hata hivyo, Mung’ong’o ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), aliipongeza Serikali kwa hatua yake ya kusimamisha baadhi ya viongozi wa Bohari ya Dawa (MSD) ili kupisha uchunguzi wa kadhia hiyo na kusisitiza kuwa watakaobainika washitakiwe na kuchukuliwa hatua za kiutendaji ili lisijirudie.

“Pamoja na hatua hizo, Kamati yetu inaishauri Serikali itoe tamko katika mkutano wa Novemba wa Bunge kuhusu suala hili na kuainisha hatua zote ilizochukua ili kuwahabarisha Watanzania walioanza kupoteza imani na dawa hizo,” alisema.

Alisema Kamati inalaani wafanyabiashara kuingiza dawa bandia nchini ili kujinufaisha bila kujali madhara kwa watumiaji na kutaka sakata hilo la ARVs liwe fundisho kwa wafanyabiashara wa aina hiyo.

TPI yakana Wakati huo huo, Uongozi wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), umekana kuzalisha ARVs bandia na kutaka waliohusika na udhalimu huo wachukuliwe hatua kali kwa sababu ni wauaji.

TPI pia imesema haijapokea barua kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya kuitaka kusitisha uzalishaji wa dawa ya aina yoyote ili kupisha uchunguzi na kudai imepokea barua kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) iliyowafikia juzi ikiwapa siku 14 za kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TPI, Zarina Madabida alisema dawa hizo bandia hazikutengenezwa na kiwanda hicho na zinazotengenezwa na kiwanda hicho ni kimuundo, nembo na hata vifungashio. Kutokana na hali hiyo, Madabida alisema anatilia shaka kuwapo mchezo mchafu wa kukiharibia kiwanda chake.

Tofauti ya bandia na halisi Alisema nembo iliyo kwenye dawa bandia za ARVs ni TT-VR30 wakati dawa halisi ambazo zinatengenezwa na TPI nembo yake ni TT-VIR30.

Pia vifungashio alisema ni tofauti ambapo wao wamekuwa wakitumia chupa nyembamba na hata rangi yake imepauka ikilinganishwa na bandia. “TFDA haijatuonesha sampuli walizokamata, ila wametuletea picha ya dawa hizo, hata kwa macho ya mtu asiyejua kusoma lazima ataona tofauti.

“Nimeambiwa vifungashio ni tofauti, kwani dawa bandia zimewekwa kwenye chupa pana, zisizo na shingo na kifuniko kipana wakati chupa tunazotumia ni nyembamba zenye shingo na mfuniko mwembamba,” alisema.

Akizungumza huku akionesha utofauti wa dawa hizo, Madabida alisema teknolojia ya kiwanda chake waliyochukua Thailand ni ya kutengeneza dawa za vidonge vya kapsuli (vyenye umbo la yai) na vyenye rangi nyeupe na si vya duara ambavyo vinatoa tabaka za rangi za dawa zilizotumika- nyeupe na chungwa.

“Teknolojia iliyotumika kutengenezea dawa bandia kwenye kiwanda chetu haipo na sisi hatuwezi kusambaza dawa ambazo hatuzalishi kwenye kiwanda chetu. Dawa hizo hazikukutwa kwenye kiwanda chetu, hivyo ni dhahiri aliyefanya hivyo alikuwa na dhamira mbaya kwa Watanzania.

“Ni kitu ambacho hakiingii akilini mtu uzalishe bidhaa wewe peke yako halafu ujitengenezee tena bidhaa bandia! Sisi ni ndio pekee tunaotengeneza ARVs nchini, hivyo tusingeweza kuzalisha kitu bandia. Mara ya mwisho kuiuzia MSD dawa ni Machi na Aprili mwaka jana, iweje hizo bandia zikutwe Agosti mwaka huu, tena Tarime?” Alihoji.

Alisema tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho ambacho kina ubia na Serikali yenye hisa asilimia 40, wamezalisha dozi milioni 2.28 za ARVs na kuhoji iweje leo wazalishe dawa hizo bandia za dozi 8,000.

Madabida alisema baada ya Agosti 6 kupokea malalamiko kutoka TFDA ya kupatikana kwa dawa bandia, walikutana na Mamlaka husika na kukubaliana kuwa wakati suala hilo linachunguzwa, dawa hizo ziondolewe kwenye mzunguko kwa lengo la kunusuru watumiaji.

Alisema pamoja na makubaliano hayo, lakini mpaka Agosti 28 hakuna kilichofanyika jambo ambalo TPI iliamua kuiandikia Mamlaka hiyo barua ya kuwakumbusha hatua hiyo.

“Wana malengo yasiyo mazuri kwetu, na wanajua tuko katika mchakato wa kupata kibali cha WHO (Shirika la Afya la Kimataifa) ambapo tutafanya biashara ndani na nje ya nchi. Hatutaacha jiwe lolote lirushwe mpaka hapo wahalifu wakamatwe na haki itendeke,” alisema.

Wizara yakomaa Ofisa Habari wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alipoulizwa, alisema Waziri hawezi kusema wamekifungia kiwanda bila kuwaandikia barua. “Sisi tumepeleka barua kama haijamfikia hilo ni jambo lingine.”

Hata hivyo, Mwamwaja alisema hana uhakika kama barua kutoka TPI imeshamfikia Waziri, kwa sababu yuko nje ya ofisi na kusisitiza kuwa suala la kukana dawa bandia linafanyiwa uchunguzi na hivyo hayuko tayari kulizungumzia.

Juzi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alitoa agizo la kukifungia kiwanda hicho kuzalisha aina yoyote ya dawa ili kupisha uchunguzi wa vyombo vya usalama kuhusu uzalishaji wa dawa bandia.

Kuwapo kwa dawa bandia za ARVs kulibainika Agosti kwenye Hospitali ya Tarime, huku Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi likidai kuwa dawa hizo zimesambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tofauti na kauli ya Serikali kuwa ni Tanga, Iringa na Mwanza. Kutokana na hali hiyo, Baraza hilo liliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

No comments:

Post a Comment