Tuesday, October 9, 2012

Nagu naye chali CCM

ILE methali ya mwosha huoshwa imejidhihirisha mkoani Manyara katika mwendelezo wa uchaguzi wa CCM na jumuiya zake.

Hali hiyo imejitokeza kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu, ambaye hivi karibuni ‘alimwosha’ Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye katika uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Wakati maji hayajakauka katika mwili wa Sumaye ambaye juzi alilalamikia uchaguzi huo kugubikwa na rushwa, Dk Nagu naye ‘ameoshwa’ katika kinyang’anyiro cha kutetea nafasi aliyokuwa nayo ya ujumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia mkoa wa Manyara.

Katika uchaguzi huo kati ya kura halali 391 zilizopigwa, Dk Nagu alipata 139 huku mpinzani wake, Martha Umbulla ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Manyara, akiibuka kidedea kwa kupata kura 252.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita, msimamizi wa uchaguzi huo, Ndengasso Ndekubali ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Mkoa, alisema katika uchaguzi huo, kura tisa ziliharibika.

Katika uchaguzi huo wa ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Hanang, ambako Nagu aliibuka kidedea dhidi ya Sumaye, kati ya kura 1,129 zilizopigwa, alipata kura 648 dhidi ya 481 za Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Akizungumza Dar es Salaam juzi na waandishi wa habari, Sumaye alidai kuwa kilichomwangusha katika uchaguzi wa NEC, ni rushwa aliyoiita ya mtandao.

Alidai kuwa uchaguzi huo uliompa Dk Nagu ushindi, uligubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho, uharamia, kuhamishwa kwa wapiga kura usiku na maovu mengine.

Katika uchaguzi wa ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Anna Jorojiki alishinda kwa kupata kura 199 dhidi ya Bahati Moses aliyepata kura 150.

Ndekubali alisema pia aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara kati ya mwaka 2005 na 2010, Dora Mushi, alimwangusha Elizabeth Malley katika nafasi ya Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa, akitetea nafasi hiyo baada ya kuishikilia kwa miaka 10.

Alisema kati ya wanachama wa UWT 400 waliopiga kura za kuchagua Mwenyekiti wa UWT Mkoa, wanachama 17 kura zao ziliharibika na kati ya kura halali 383 zilizopigwa, Mushi alipata 238 na Malley 145.

Akizungumza na waandishi baada ya kushinda nafasi hiyo, Umbulla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, alishukuru wanachama wa UWT kwa kumchagua na kuwataka wavunje kambi na vikundi ili kupanua wigo wa kujenga na kudumisha chama.

Alisisitiza, kwamba hakuna mbinu yoyote aliyotumia kumshinda Dk Nagu ila wanawake hao walikumbuka mambo aliyoyafanya kwenye nafasi yake.

Alisema wanawake wa Manyara wanajua nini amewafanyia kupitia nafasi yake ya ubunge wa viti maalumu na aliwashukuru kwa kumwona kuwa anafaa kwani asingewaelewa wasingemchagua.

No comments:

Post a Comment