Wednesday, September 19, 2012

I-View Studio kurekodi Video mpya ya Diamond Platnumz


KAMPUNI I-View Studios ya mjini Dar es Salaam imeshinda mchakato wa kurekodi video mpya ya msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambayo usaili wake utafanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge, Dar es Salaam.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole alisema I-View imepata nafasi hiyo kutokana na kiwango kikubwa cha video kadhaa ilizofanya lakini pia vifaa ilivyo navyo na uwezo wa wafanyakazi wake.
“Siku zote kila mtu anaangalia kitu kizuri, Diamond ametaka kufanya mapinduzi katika tasnia ya muziki, lakini kufanya mapinduzi kunahusisha vitu vingi, tungo zake yeye kama msanii, studio anayorekodia watu watakaoshiriki kwenye video yake kampuni itakayorekodi video pia, lakini mwisho wa siku I-View chini ya Raqey Mohamed ndio imeshinda nafasi hiyo.

“Raqey anafahamika kwa kazi zake pamoja na kurekodi matangazo mbalimbali ya Televisheni, picha mnato lakini pia video za wasanii Taznim ya Kwasakwasa, Utanikumbuka ya Suma Lee ni baadhi ya kazi ambazo zinaonyesha uwezo alionao lakini pia Diamond na timu yake tumeweza kuona vifaa vipya na vya kisasa ambavyo Raqey anavyo kwa sasa na hakuna kwa Afrika Mashariki na Kati,” alisema.

Kwa upande wake Raqey ambaye ni Mkurugenzi wa I-View alisema anahitaji kuifanya kazi hiyo kuwa tofauti ili kusukuma mbele sekta ya mawasiliano na muziki kwa ujumla.
“Sisi kama I-View tunafurahi kufanya kazi na Diamond, ni msanii mzuri na mkubwa ambaye kazi zake zinaonekana, hatutamuangusha na mashabiki na wasanii wengine wasubirie kazi itakapotoka,” alisema.

I-View pia watashiriki katika mchakato wa kupata watu watakaonekana kwenye video hiyo ambayo ni kwa mara ya kwanza nchini kutafanywa usaili wa washiriki. Usaili huo utafanyika Jumamosi katika ukumbi wa Nyumbani Lounge ambao unamilikiwa na mwanamuziki Lady Jaydee. Majina ya majaji wataochuja yatanatarajiwa kutangazwa leo.

No comments:

Post a Comment