TAKRIBANI wanafunzi 97 wa sekondari ya Seeke, wilayani Kahama mkoani Shinyanga hawatafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne, kutokana na kukosa fomu za maendeleo ya mwanafunzi akiwa shule ya msingi (TSM 9).
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wanafunzi hao wakisubiri kuingia katika vyumba vya mitihani. Wakizungumza na gazeti hili, wanafunzi hao walidai fomu hizo walizijaza na kulipa ada ya mitihani na kuongeza kuwa wanashangaa kuona jana wakizuiwa kuingia chumba cha mtihani.
“Aliitwa Mwalimu Mkuu Msaidizi, Daniel Mtuli ambaye alitaja majina ya wanaotakiwa kufanya mtihani huku wengine wakiachwa katika orodha hiyo,” alidai mmoja wa wanafunzi hao.
Alidai katika orodha hiyo, wanafunzi 53 waliochaguliwa kuingia katika chumba cha kufanyia mitihani kati ya wanafunzi 150 wanaotakiwa kufanya mitihani hiyo hali ambayo ilisababisha wanafunzi 97 kutofanya mtihani huo jana.
“Mimi nina siku nne tangu nikabidhiwe ofisi hii na Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kahama, Joseph Gwasa na nilipokabidhiwa, nilipewa maelekezo kuwa ni wanafunzi 53 ndio wanaopaswa kufanya mtihani huo wa kidato cha nne,” alisema Mtuli alipohojiwa kuhusu utata huo.
Mtuli alisema Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Maduhu alisimamishwa kazi katika shule hiyo tangu Oktoba 3 kwa sababu hizo hizo.
Alielezea kusikitika kuona wanafunzi hao wakipoteza muda wao wa miaka minne na kuambiwa jana kuwa hawawezi kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya sekondari.
Wanafunzi hao walipofika katika ofisi ya Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya, kujua hatima yao ya kufanya mitihani, hawakuonana naye kwa madai kwamba alikuwa na kazi nyingi.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao waliamua kuandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya kupinga kitendo cha kuzuiwa kufanya mitihani. Juhudi za kumpata Mpesya kwa njia ya simu ili kujua hatma ya wanafunzi hao, zilishindikana kwa kuwa simu yake ilikuwa haipatikani.
Wakati hayo yakitokea Shinyanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Joyce Ndalichako, alisema mitihani hiyo ya kidato cha nne, ilianza vizuri bila matatizo na wanafunzi hao jana walianza na masomo ya Uraia na Kiingereza.
“Ni mapema mno kuzungumzia hali halisi, lakini mpaka sasa mambo ni mazuri ingawa baadaye kupitia taarifa za wasimamizi, tunaweza kukuta taarifa za udanganyifu na mambo mengine ya changamoto,” alisema Dk Ndalichako.
Gazeti hili lilitembelea baadhi ya shule za Dar es Salaam zikiwamo za Salma Kikwete, Manzese, Jitegemee na Makongo na kukuta wanafunzi wakifanya mitihani yao kwa utulivu huku wasimamizi wakidai kutokuwapo na mushkeli wowote.
Hata hivyo, katika sekondari ya Manzese Mkuu wa Shule, aliyekataa kutaja jina lake aliwajia juu waandishi wa habari kwa kuingia ndani ya shule hiyo na kuhoji hali ya mitihani huku akidai kuwa hiyo si kazi yao kama wanataka kujua wakamwulize Ndalichako.
“Nasema hivi, mimi sijui mmefuata nini? Mnaniuliza mimi kwani mimi ndiye nafanya mtihani, kasubirini huko kwa Mkurugenzi wa Elimu au kwa Ndalichako hapa hamruhusiwi,” alisema kwa jazba.
No comments:
Post a Comment