October 29 mwaka huu tuliandika habari yenye kichwa cha habari, “Mpwa wa Bi. Kidude aishutumu Sauti za Busara kwa kumtelekeza shangazi yake” ambapo mpwa wake huyo aliongea na kipindi cha Mimi na Tanzania kinachooneshwa na kituo cha runinga cha Channel Ten.
Tuliahidi kuwa tutafanya jitihada za kuutafuta uongozi wa Busara Promotions ili ulieleze suala hili kwa upande wake. Tunashukuru kuwa uongozi huo umetujibu kupitia mwakilishi wake Journey Ramadhan kama ifuatavyo:
Ni matumaini yetu umzima na unaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa kama
kawaida. Nianze kwa shukrani na pongezi kwako hasa kwa jitihada zako kufuatilia hili
suala kwa kina ikiwa ni mhariri wa kwanza (mhariri bongo5) kufanya jitihada za kutaka kujua ukweli tangu suala hili litolewe kwenye vyombo vya habari.
Kuna stori ndefu sana kati ya Bi Kidude na Sauti za Busara, nimeambatanisha
nakala ambayo ina historia fupi tu kati ya Bi Kidude na Sauti za Busara,
lakini nafasi hii nitatoa maelezo kutokana na shutuma zilizotolewa na mpwa
wa Bi Kidude dhidi ya Sauti za Busara.
Yusuf Mahmoud alijitolea kuhifadhi pesa ya Bi Kidude baada ya kuona
usimamizi usioridhisha katika haki zake, katika uhifadhi huo walikubaliana
Bi Kidude awe anachukua pesa zake kutokana na mahitaji yake ya kila siku,
tena kwa maandishi.
Katika mfululizo wa kuchukuwa pesa zake alikuwa anachukua kiasi tofauti ambapo muda mwingine anaweza kuchukua kiasi kikubwa cha pesa lakini baada ya muda si mrefu pesa inamalizika, baada ya kuona hivyo mjukuu wa Bi Kidude akashauri apewe elfu 50,000 kila wiki. Sauti za busara inatoa malipo ya Bi Kidude ya matibabu au kama kuna ujenzi nyumbani kwake na gharama nyingine kutoka katika pesa ya Bi Kidude mwenyewe.
Bi Kidude kabla ya kuhamishiwa shamba kwa mpwa wake alikuwa anakuja
kuchukuwa pesa zake mwenyewe kila wiki, na baada ya kuhamishiwa shamba
kutokana na maradhi Mpwa wake alikuwa anakuja kuchukuwa pesa ya Bi Kidude ya
kila wiki, na kabla ya kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu bili ya
matibabu ililipwa na Sauti za Busara ingawa hatukupewa taarifa kama Bi
Kidude anapelekwa Dar es Salaam kwa matibabu.
Kwa hiyo Sauti za Busara inapinga kauli ya mpwa wa Bi Kidude inayosema Sauti
za Busara imemtelekeza Bi Kidude, tumeshampigia simu mara nyingi ili
wazungumze hili suala kifamilia kwa sababu Sauti za Busara inataka kukabidhi
pesa ya Bi Kidude hata leo lakini lazima apatikane mtu ambaye atachaguliwa
na familia, lakini tatizo lililopo sasa wanafamilia wenyewe hawajakubaliana
nani apewe hizo pesa.
TAARIFA RASMI KUTOKA BUSARA KUHUSU BI KIDUDE
Busara Promotions ni taasisi isiyokuwa ya kibiashara ambayo ilianzishwa mwaka 2003 zanzibar.
Mahusiano kati ya Busara Promotions na Bi kidude yalianza mwaka 2005 kipindi ambacho Bi kidude alipopata tuzo ya Womex, Yusuf Mahmoud ambaye ni Mkurugenzi wa Busara Promotions alikuwepo katika kamati ya uteuzi ya mshindi na ndie alipendekeza jina la Bi kidude kupewa tuzo hiyo ambayo ilikuwa inawaniwa na wanamuziki mbalimbali maarufu duniani kama Peter Gabriel -Uingereza, Mariam Makeba –Afrika Kusini, Djanan Gasparan –Urusi.
Yusuf Mahmoud alishikilia msimamo wake wa kumchagua Bi Kidude ingawa alipata wakati mgumu kutoka kwa wana kamati wenzie ambao walikuwa wanamuuliza ni kwasababu gani amempendekeza Bi Kidude ambaye naye aliwajibu kwamba kuna sababu nyingi za kumpendekeza Bi Kidude kwanza Bi Kidude ni msanii mkongwe ambaye bado anaendeleza ngoma za utamaduni ikiwemo taarabu asilia, pili ni msanii pekee mkongwe wa Zanzibar, ingawa watu wengi walimpigia kura Mariam Makeba. Mwishowe Bi Kidude alifanikiwa kupata Tuzo hiyo.
Tuzo hiyo ilitolewa na kiasi cha pesa euro 5,000 lakini kutokana na sheria ya Tuzo mshindi huwa hakabidhiwi pesa mkononi ila hupendekeza ile pesa isaidie nini katika nchi yake na hupelekwa sehemu inayohusika. Yusuf Mahmoud alijaribu kuelezea hali ya maisha ya Bi Kidude kwamba hana nyumba nzuri, benki akaunti nk, kwahiyo akapendekeza ile pesa itumike katika matengenezo ya nyumba yake.
Kwakuwa sheria ilikuwa haisemi hivyo ikabidi vianze vikao na viongozi wa Womex ili watoe mawazo yao katika suala hilo, baada ya vikao kadhaa wakakubaliana wampe pesa nusu ambayo ilikuwa euro 2500 kuendeleza ujenzi wa nyumba na nusu yake iwe inamsaidia mwenyewe kwa matumizi yake ya kila siku.
Katika makubaliano yao viongozi wa Womex walihitaji picha za ujenzi wa nyumba ili wajiridhishe na makubaliano yao.
Kwakuwa hakuwa na akaunti ya benki Yusuf Mahmoud alimsaidia kumtunzia pesa zake ambazo huzichukua tu pindi anapokuwa na mahitaji nazo. Yusuf Mahmoud aliendelea kumtunzia pesa zake ambapo kuna Folder la Bi Kidude peke yake la tangu mwaka 2005 mpaka sasa likiwa na rekodi ya pesa inayoingia na inayotoka.
Kuna kipindi Yusuf alikwenda kwenye tawi la benki ya FBME kipindi hicho meneja wa tawi alikuwa ndugu Nasor Rajab Dachi kwa ajili ya kumfungulia akaunti ya benki ambapo ndugu Dachi alikubali kumsaidia Bi Kidude kuandika pindi atakapotaka kutoa pesa zake lakini kwa bahati mbaya Bi Kidude mwenyewe alikataa, na alikataa kwa sababu alishawahi kufanya maonyesho nje ya nchi na pesa zake zikawa zinatumwa kwa njia ya western union kuna mtu alikuwa anakwenda kumchukulia na pesa ikawa haimfikii ndio maana alikataa mambo ya benki. kwahiyo pesa zake zote za maonyesho ambayo yanasimamiwa na Yusuf ilikuwa inafikia Busara Promotions.
Katika kuelezea hili naomba umma wa watanzania waelewe kwamba si kila onyesho analofanya Bi Kidude basi Busara Promotions inahusika ameshafanya maonyesho mengi ndani na nje ya nchi lakini Busara Promotions haijashirikishwa. Karibu miaka yote ya Tamasha la Sauti za Busara Bi Kidude ameshiriki isipokuwa mwaka 2010 ambapo alitangazwa katika wasanii watakaofanya onyesho lakini kwa bahati mbaya alikuja kuchukuliwa kwa ajili ya onyesho la mradi wa malaria jijini Dar es Salaam ambapo ikumbukwe maonyesho yote ya Dar es salaam na mikoani Sauti ya Busara haijawahi kushirikishwa kwa namna yoyote ile.
Mwaka huu Bi Kidude alikwenda Poland kwaajili ya onyesho ambalo lilisimamiwa na Sauti za Busara lakini aliporudi tu Baraza la Sanaa Zanzibar nalo likamchukua kwa ajili ya safari ya Komoro ambapo Sauti za Busara haikushirikishwa kwasababu mara nyingi Bi Kidude anapokuwa anataka kusafiri huwa anagewa muda wa kupumzika kwa ajili ya safari.
Baadhi ya watu wa Baraza walikwenda kwa familia ya Bi Kidude ambapo waliahidiwa kupatiwa pesa atakaporudi wakamruhusu kwenda Komoro. Baraza likawasiliana nasi na wakasema wanamchukua Bi Kidude ila pesa yake italetwa atakaporudi lakini kwa bahati mbaya pesa haikuletwa.
Aliporudi safari ya Komoro afya yake ilikuwa sio nzuri hasa kutokana na uchovu na kutumia muda mwingi bila ya kupumzika.
Miaka yote hiyo Bi kidude anakuja kuchukua pesa yake mwenyewe kutokana na mahitaji yake lakini Yusuf na baadhi ya wanafamilia yake wakasema inabidi aje kuchukua elfu 50,000 kila wiki. Mwaka huuhuu ndio alikuja na Bwana Baraka ofisi za Sauti za Busara akamtambulisha kwetu na akasema “kuanzia sasa Baraka ndio atakuwa anakuja kuchukua pesa yangu ya kila wiki 50,000”. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kumjua Baraka Abdallah, alikuwa anakuja kuchukuwa pesa za kila wiki 50,000.
Cha kushangaza tukasikia kwa watu kwamba Bi Kidude ameonyeshwa kwenye televisheni ya Zanzibar (ZBC) anaumwa sana na hakuna mtu yeyote wa Sauti za Busara anayekwenda kumuangalia wala kutoa msaada wake na Baraka Abdallah akaonyeshwa kwenye kipindi hicho.
Tukawasiliana na Baraka Abdallah kuhusu hilo suala yeye akasema “kweli walikuja watu wa kuhamasisha sensa ila mimi nimewaambia Bibi hawezi kufanya onyesho wala tangazo lolote kwa sasa” tukafanya jitihada za kuwasiliana na kaka yake Bi Kidude yeye akasema mimi sijui lolote kwa sababu Bi Kidude amehamishwa hapa kupelekwa Bububu wakati sijui na wala sijashirikishwa katika hilo.
Tarehe 31/07/2012 tukapokea barua kutoka Baraza la sanaa Zanzibar la kututaka sisi tufike kwenye mkutano na dhumuni la mkutano kuhusu kusimamishwa kufanya maonyesho Bi Kidude na lingine maombi ya wana familia wanataka haki zote za Bi Kidude zisimamiwe na Baraza.
Mkutano ulikuwa tarehe 7/08/2012 kwa bahati nzuri kaka na mjukuu wa Bi Kidude walihudhuria ambapo kwanza kaka wa Bi Kidude alisema huo sio msimamo wa familia huo ni msimamo wake binafsi na amefanya hivyo ili ajinufaishe yeye kupitia pesa za dada yangu. Katika mkutano Yusuf alishakuwa tayari kukabidhi zile pesa kwa familia lakini kutokana maelezo ya kaka wa Bi Kidude Baraza la Sanaa walishauri kwanza Yusuf aendelee kuhifadhi pesa ya Bi Kidude mpaka watakapomuandikia barua Baraka ili wakae kwa ajili ya kujadili kwa kina suala hilo.
Lakini kwa bahati mbaya hakupata barua kutoka Baraza la sanaa Zanzibar kwa ajili ya kulizungumzia suala hilo.
Kuna siku Bi Kidude alipita ofisini akitokea hospital akasema “pesa sijapewa au Baraka haji kuchukua?” akajibiwa “Baraka anakuja kuchukua kila wiki”
Bi Maryam ni mtu wa karibu sana na Bi Kidude na mtu ambaye alishakaa na Bi Kidude takriban miaka minane, Bi Maryam alikwenda kumchukua Bi Kidude baada ya kusikia kuwa hali yake sio nzuri, aliwasiliana nasi kututaarifu tukaenda kumtazama hospitali ya Zanzibar Medical Group.
Huduma ziliendelea pale Hospitali kwa kuwa Bi Kidude alipatiwa kitanda na akatakiwa apumzike, Bi Maryam ndiye aliyekuwa anampelekea chakula Bi Kidude kwa sababu alielekezwa na Daktari kwamba anahitaji lishe bore, Yusuf alichangia pesa ya chakula tofauti na akiba ya Bi Kidude na kumpatia Bi Maryam.
Kuna siku tukapokea simu kutoka kwa Bi Maryam anasema “nimepigiwa simu na Daktari wa Bi Kidude ameniambia kuna jamaa zake Bi Kidude wanafanya zogo hospital wanamtaka Bi Kidude” Yule Daktari akamwambia Bi Maryam kwamba yeye anawaruhusu wamchukue Bi Kidude na kuhusu bili yake Bi Maryam akamwambia yule Daktari kwamba Sauti za Busara watakuja kulipa. Siku hiyo Bi Kidude alichukuliwa na kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Sisi tukaenda kulipa ile bili iliyogharimu shilingi 270,000 lakini ikumbukwe Bi Kidude amechukuliwa hata ya sisi kutaarifiwa, na Busara wasingeweza na hawawezi kumzuia Bi Kidude asiende kufanyiwa matibabu kwa sababu Sauti za Busara inapenda kumuona Bi Kidude akiwa na afya njema.
Aliendelea na matibabu Dar nasi tukawa tunapiga simu kwa ajili ya kuulizia hali yake alivyorudi kutoka Dar tukaenda kumuangalia, kuna siku tulikwenda kumuangalia lakini kwa bahati mbaya Baraka Abdallah hakuwepo na kila tulipokuwa tunakwenda tunampelekea pesa yake. kuna siku tulikwenda tukamkuta Baraka akatuelezea hali ya Bi Kidude kwamba sasa na utu uzima nao unachangia kwa sababu muda mwingine anapoteza kumbukumbu na kuongea suala moja hata mara tatu.
Katika mazungumzo akasema anataka kumpeleka Bi Kidude Hopsitali ya Taifa, Mnazi mmoja tukamwambia basi atujulishe na aje kuchukua pesa akakubali. Baada ya siku kufika akapigiwa simu akakataa kuja. Na tumeshapigia simu si mara moja wala mara mbili kwamba aje na aseme anataka nini lakini hatokei, inasemekana anataka pesa yote ya Bi Kidude. Yusuf yupo tayari hata sasa hivi kukabidhi pesa yote ya Bi Kidude lakini familia bado inakinzana katika suala hilo ambapo kaka wa Bi Kidude anakataa.
Familia bado inavutana kwa sababu baadhi ya wana ndugu wanamtuhumu Baraka kwamba anataka kumfanya Bi Kidude kama mtaji na ndio maana amemchukua nyumbani kwake. Sauti za Busara haitaweza kuingilia mgogoro wa familia kuhusu pesa ya Bi Kidude ila ipo tayari hata sasa hivi kukabidhi pesa yote ya Bi Kidude kwa mtu ambaye atachaguliwa na wana familia.
Sauti za Busara haina kinyongo na Baraka wala familia ya Bi Kidude ila tunachoshangaa ni kwanini hataki kuja ofisini ili aelezwe stori nzima ya mahusiano kati ya Yusuf na Bi Kidude kwani inafahamika ni mtu ambaye amejitokeza kipindi hiki cha hivi karibuni na hajui stori ya Bi kidude na Sauti za Busara na badala yake kukimbilia kwenye vyombo vya habari kueleza vitu ambavyo hana uhakika navyo.
Tunatoa wito kwa vyombo vya habari vyote nchini mlango upo wazi wanakaribishwa ili wapate taarifa rasmi kuhusu Bi Kidude.
No comments:
Post a Comment